Header Ads

MKUU WA MAJESHI AZIMA MAPINDUZI YA KIJESHI NCHINI BURUNDI

Baada ya masiku kadhaa ya machafuko ya umwagaji damu yaliyojiri katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, Meja-Jenerali Godefroid Niyombare, afisa wa ngazi ya juu wa jeshi ametangaza kupitia redio moja ya binafsi kuwa mapinduzi ya kijeshi yamefanyika nchini humo. Jenerali Niyombare amesisitiza kuwa Rais Pierre Nkurunziza ameondolewa madarakani na baraza lake la mawaziri limevunjwa. Wakati huohuo Mkuu wa majeshi ya Burundi Jenerali Prime Niyongabo ametoa tamko jengine kupitia redio ya serikali na kuwatangazia wananchi kwamba mapinduzi hayo ya kijeshi yamezimwa. Jenerali Niyongabo amewahakikishia wananchi kuwa wanajeshi watiifu kwa Rais Nkurunziza wameidhibiti Ikulu ya Rais pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura. Mbali na utata huo, kuna habari za kutatanisha pia kuhusu mahali aliko Rais Pierre Nkurunziza mwenyewe. Jana Jumatano, kiongozi huyo alikuwa ameelekea Dar es Salaam, Tanzania kuhudhuria kikao cha dharura cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); na kwa mujibu wa ripoti za mwisho ni kwamba angaliko mjini Dar es Salaam. Nayo serikali ya Uganda imekanusha habari za kuwasili nchini humo Rais wa Burundi kupitia bandari ya Entebe. Kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi lilikuwa jambo la kutarajia kutokana na hali ya mgogoro inayoshuhudiwa hivi sasa nchini humo. Japokuwa tangazo la jeshi la kutopendelea upande wowote kati ya pande hasimu kwenye mgogoro wa nchi hiyo na kimya kilichoonyeshwa na makamanda wa jeshi katika muda wote wa mwezi mmoja sasa vilipunguza uwezekano wa kutokea mapinduzi hayo. Kutokea mapinduzi ya kijeshi kulizidi kuonekana kuwa ni jambo lililo mbali kutokana na hitilafu za mitazamo pia zilizojitokeza kati ya maafisa wa polisi na makamanda wa ngazi za juu wa jeshi. Pamoja na hayo kuondoka nchini Rais Nkurunziza na kuelekea Tanzania kwa safari rasmi kulitoa fursa kwa majenerali wa jeshi ya kuchukua hatua dhidi yake.Meja-Jenerali Niyombare, ambaye mwezi Februari alivuliwa wadhifa wake wa Mkuu wa Idara ya Intelijinsia na Usalama wa nchi, alishirikiana na baadhi ya maafisa waandamizi wa jeshi na polisi na kufanya mapinduzi ya kijeshi. Msimamo wa jenerali huyo wa kupinga uamuzi wa Rais Nkurunziza wa kugombea urais kwa muhula wa tatu ndio uliomponza na kumfanya avuliwe wadhifa aliokuwa nao. Tunaweza kusema kuwa uamuzi wa Nkurunziza wa kutaka aendelee kuwa rais wa Burundi baada ya kuweko madarakani kwa kipindi cha miaka kumi umeigawa nchi hiyo katika kambi mbili za wapinzani na waungaji mkono wa uamuzi wake huo. Mgawanyiko na mpasuko huo ndani ya jamii ya Burundi ulianzia katika vyama na makundi ya kisiasa na kudhihirika zaidi hivi sasa kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi ambalo limewagawa pia makamanda wa jeshi na vikosi vya usalama vya nchi hiyo. Msimamo wa Rais Pierre Nkurunziza wa kutaka aendelee kuwania urais kwa muhula wa tatu ulipingwa na kukosolewa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya pamoja na nchi nyingi za Kiafrika. Pamoja na hayo kutokana na kuungwa mkono na viongozi wa chama chake tawala cha CNDD-FDD na bila kujali maandamano ya kumpinga ya wafuasi wa vyama vya upinzani yaliyoutikisa mji mkuu Bujumbura, alishikilia msimamo wake huo wa kugombea tena urais. Hata vifo vya watu wasiopungua 23 waliouawa katika machafuko na maandamano ya upinzani havikuiteteresha azma ya Nkurunziza ya kuwania tena urais wa Burundi. Kwa mujibu wa baadhi ya duru, mazungumzo yanayofanyika kati ya makamanda wa jeshi yanazidi kuupa nguvu uwezekano wa kuzimwa mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea jana nchini humo.
Alaa kulli hal ung’ang’anizi wa Nkurunziza wa kutaka aendelee kubaki madarakani umemtumbukiza kiongozi huyo kwenye kapu la viongozi wa kizazi kilichopita barani Afrika waliosibiwa na ugonjwa wa uchu wa madaraka, ambao hatimaye waling’olewa madarakani kwa nguvu kutokana na mashinikizo ya maandamano ya wananchi au mapinduzi ya kijeshi. Lisilo na shaka ni kuwa kutokana na hali inayoshuhudiwa hivi sasa nchini Burundi, ya kutibuka na kuvurugika hali ya usalama hakuna uwezekano uchaguzi wa tarehe 26 ya mwezi ujao wa Juni kufanyika kama ulivyopangwa. La kusubiri ni kuona radiamali gani itatolewa na viongozi wa Umoja wa Afrika na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusiana na matukio yanayoendelea kujiri nchini Burundi…/

Hakuna maoni